Tanesco yataja ukame kuwa sababu ya kukatika umeme

by rumulifm

Kutokana na ukame, Tanesco imesema mabwawa ya kuzalisha umeme ya Hale, Kihansi, Nyumba ya Mungu na Pangani yenye uwezo wa kuzalisha megawati 266 za umeme sasa yanazalisha megawati 34 tu.

Dar es Salaam. Shirika la Umeme (Tanesco) limesema ukame unaoikabili nchi ndiyo sababu kubwa ya changamoto ya ukatikaji wa umeme wa mara kwa mara unaoendelea nchini.

Hayo yameelezwa jana Oktoba 30 na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Shirika hilo, Martin Mwambene.

Mwambene amesema mabwawa ya kuzalisha umeme ya Hale, Kihansi, Nyumba ya Mungu na Pangani yenye uwezo wa kuzalisha megawati 266 za umeme sasa yanazalisha megawati 34 tu.

Ameitaja iliyoathirika kwa kiasi kikubwa kutokana uzalishaji mdogo kuwa pamoja na Arusha, Kilimanjaro na Tanga.

 “Kutokana na ukame huu mkubwa, mikoa hiyo inalazimika kupata umeme wake kutoka katika vituo vya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia vilivyopo Dar es Salaam,” amesema.

Aidha amesema kutokana na kuongezeka kwa kasi ya shughuli za uchumi na viwanda katika mikoa hiyo njia za kusafirisha umeme kutoka DSM kwenda kwenye mikoa tajwa zimezidiwa jambo linalosababisha umeme unaopatikana kutoka mikoa hiyo kutokidhi mahitaji.

Mwambene ameeleza ili kutatua changamoto hii, shirika limechukua hatua ya kujenga njia mpya kutoka kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Luguruni jijini Dar es Salaam ili kuhudumia maeneo yote hadi Chalinze, ili kutoa nafasi ya umeme mwingine kufika katika mikoa hiyo.

“Hii itasaidia kupunguza mzigo wa umeme katika njia ya sasa inayotoka Ubungo hadi Chalinze na hivyo kuruhusu umeme mwingi kwenda katika mikoa tajwa,” amesema.

Kujenga njia mpya kutoka kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Lemugrul kilichopo Kisongo jijini Arusha.

“Hatua hii itapunguza mzigo wa umeme unaopita kwenye kituo cha Njiro hivyo kuongeza kiasi kingine cha umeme kufika mikoa ya Kilimanjaro na Tanga,” amesema.

Pia ameeleza hali ya ukame iliotabiriwa kutokea mwaka huu shirika limechukua hatua za kuongeza uzalishaji wa umeme kupitia vituo vyake vya gesi ambapo katika upanuzi wa kituo cha Kinyerezi 1 imefika ukingoni na wanatarajia kuingiza megawati nyingine185 katika gridi ya Taifa.

“Megawati 90 kati ya hizo zipo kwenye majaribio, nakusema hatua hii itaimarisha uwezo wa kukabiliana na upingufu wa maji ambao unaendelea,”

Aidha Mwambene amesema pamoja na kazi zote hizi kuendelea kufanyika, Ofisi zao zote za mikoa zitaendelea kutoa ratiba ya upungufu wa umeme kwenye maeneo yote yanayoathirika.

“Wateja wetu watapewa taarifa kwa njia mbalimbali zikiwemo pamoja na ujumbe mfupi wa meneno kwenda kwa mhusika wa eneo hilo lililoathirika,” amesema.

You may also like

Leave a Comment

We use cookies on our website to give you the most relevant experiences. By clicking “Accept”, you consent to the use of all the cookies Accept